Coronavirus: Idadi ya walioambukizwa virusi vya corona yaongezeka Tanzania

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa
Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa wa corona baada ya watu wengine wawili kuthibitishwa visiwani Zanzibar na Dar es Salaam. Wagonjwa wote ni raia wa kigeni.

Siku ya Jumanne nchi hiyo ilitangaza kufunga shule zote kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.

Serikali imethibitisha hayo baada ya wagonjwa hao wawili kufanyiwa vipimo vya maabara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Sampuli ya kwanza ni ya mwanaume,raia wa Marekani, 61 ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.

Mgonjwa huyu ametengwa katika sehemu maalumu kwa ajili ya taratibu nyingine za kitabibu, pia ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu naye.

Zanzibar kwa upande wake imesema sampuli ya pili iliyopokelewa kutoka Zanzibar, ni ya mwanaume mwenye umri wa miaka 24, raia wa Ujerumani.

Taarifa kumhusu zitatolewa baadae na Waziri wa Afya wa Zanzibar.

Hapo jana Waziri Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule zote kuanzia za awali mpaka kidato cha sita kwa siku 30 zikiwa ni jitihada za kudhibiti maambukizi.

Wizara itafanya marekebisho ya ratiba kwa wale wanaotarajiwa kufanya mitihani tarehe 4 Mei, itasogezwa mbele kadiri ya matokeo yatakavyojitokeza ili nao wapate kusoma kwa kipindi kilekile kilichokubalika na ratiba hiyo.

Lakini pia serikali ya Tanzania imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama vile ligi kuu ya Tanzania, Ligi daraja la pili, ligi daraja la kwanza lakini pia michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) , michezo ya shule za sekondari(UMISETA) pamoja na michezo ya mashirika ya umma.

Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.

Aidha bwana Majaliwa alisisitiza kuwa nchi imejiandaa vyema kukabiliana na mlipuko wa COVID 19 nchini Tanzania.

Tanzania yatangaza kufunga shule zote

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tanzania yatangaza kufunga shule zote kuanzia za awali mpaka kidato cha sita

Kwa nini Tanzania imefikia maamuzi ya kufunga shule?

Hapo jana Tanzania ilithibitisha kuwa na mgonjwa mmoja wa virusi vya corona.

Mnamo tarehe Machi,15, mgonjwa huyo alisafiri kuingia Tanzania majira ya saa kumi jioni.

Mgonjwa aliyetangazwa ni mwanamke wa miaka 46 raia wa Tanzania, ambaye aliwasili kutoka Ubelgiji kwa ndege ya shirika la Rwanda.

Msafiri huyo aliondoka nchini tarehe 3,Machi 2020 ambapo kati ya tarehe 5-13 Machi alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji.

Msafiri huyo alipita uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Waziri Ummy Mwalimu amesema msafiri huyo alipofika KIA alifanyiwa ukaguzi na maafisa wa afya na kuonekana kutokuwa na homa.

Baadae alianza kujisikia vibaya akiwa hotelini na kwenda hospitali ya mkoa ya rufaa ya Mount Meru Arusha ambapo sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii iliyoko Dar es salaam kwa ajili ya uchunguzi.

"Vipimo vya maabara vimethibitisha kuwa mtu huyo ana maambukizi ya ugonjwa wa corona, covid -19, Mgonjwa anaendelea vizuri na matibabu."

Waziri Ummy ameongeza kusema," Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba ugonjwa huu unathibitiwa ili usisambae nchini.

Ramani inayoonesha maambukizi Afrika
Maelezo ya picha, Ramani inayoonesha maambukizi Afrika